Uongozi huanzia utotoni:Naibu Waziri Anna Athanas Paul

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul, amesema kuwa uongozi kwa wanawake lazima uanze katika ngazi za awali tokea watoto wakiwa shuleni ili kuwa viongozi mahari wa baadae katika kuiongoza nchi.

 Aliyasema hayo katika mkutano wa wadau na vijana wa kike wenye lengo la kuwezeshwa katika kuwania nafasi za uongozi Zanzibar, ulioandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-Zanzibar). 

 Naibu Waziri huyo aliwataka vijana kutorudi nyuma licha ya changamoto mbalimbali wanazopitia katika kuwania nafasi za uongozi na changamoto hazimrudishi mtu nyuma bali zinampa nafasi ya kusonga mbele na kujiimarisha zaidi.

 “Msiogope kuingia kwenye nafasi za uongozi na mara nyingi vijana wanakuwa woga wanapoona kuna wanaume wamesimama kwenye majimbo lakini msiogope na mnaposimama mtawapa changamoto wanaume na mwisho watatambua kama na nyie mna uwezo na elimu ya kuwania hizo nafasi” alisema.

 Alisema nafasi za uongozi zipo nyingi na sio lazima kwenye siasa na vijana wengi wamekuwa wakikimbilia kwenye uongozi wa siasa na kusahau sehemu nyengine ambazo zimejaa wanaume. 

 Naibu waziri huyo alisema wanawake makini ni wale ambao hawaogopi kuingia kwenye nafasi hata kama kuna wanaume waliojitokeza kuwania hizo nafasi muhimu wao wanachangamkia nafasi hizo na kuingia kwenye kinyanganyiro kuwania na kugombea nafasi za uongozi. 

 Alisema Rais Dk Mwinyi ameonesha mfano mzuri wa kuwainua wanawake kwa kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi hivyo hakuna sababu ya wanawake kubaki nyuma kwa kuwa wana kigezo kizuri cha kuiga. 

 “Tunao mfano mzuri wa mheshimiwa Rais wetu ametuinua sana wanawake kwa kututeuwa lakini pia jamii isiturudishe nyuma, tutumie nafasi zetu kama wanawake na tusikubali kushindwa na wanaume katika kuwainua wanawake vijana ambao wanapaswa kusimama katika nafasi za uongozi” alisema Naibu Waziri.

 Alisema TAMWA ni taasisi inayosaidia wanawake na vijana kwa muda mrefu ikiwanyanyua wanawake katika masuala mbalimbali ikiwemo ya kudai haki za wanawake, kupambana na udhalilishaji, kuwania nafasi za uongozi lakini pia kuwainua na kuwajengea uwezo nafasi za uongozi ikiwemo vijana. 

Alisema amefurahishwa na kuiona TAMWA ikifanya kazi zake kwa ufanisi khasa katika kuwachukua vijana na kuanza kuwapa elimu ya kujiamini na kujitambua ili kuwania nafasi za uongozi mapema kabla ya kumaliza vyuo na muhimu kuanza kupewa elimu mapema ni jambo zuri na la busara zaidi.

“Ni muhimu nafasi hizi za uongozi kugombaniwa kuanzia kwa vijana kwa kuanzia mashuleni na ukija katika jamii unaendeleza kwa kuwa tayari umeshapata uzoefu hivyo tujitahidini katika kuwainua vijana na vijana mhamasike” alisema Anna. Naye Mkurugenzi wa (TAMWA Zanzibar) Dk Mzuri Issa Ali alisema wazee wanamalizia umri wao katika nafasi zao hivyo zinahitaji kujazwa na vijana. 

“Vijana mnapaswa kujituma zaidi ili kuchukua nafasi za uongozi na hivi sasa wazee wanazeeka na kuondoka na nafasi hizi zinahitaji kujazwa nyinyi ndio mtatakiwa kuchukua hizo nafasi na hasa kwa kuzingatia hivi sasa tuna nafasi nzuri kwa kuwa Rais wetu wa Tanzania ni mwanamke” alisema Dk Mzuri. Akitoa ushuhuda wake Dk Mzuri alisema alianza kupenda kuandika na kutoa taarifa zinazowahusu wanawake na vijana kabla ya kujiunga na TAMWA na mwisho akajikuta amewasaidia wanawake. 

 Akizungumzia masuala ya wanawake na uongozi Dk Mzuri alisema kupitia TAMWA wametumia nafasi ya kuwajengea uwezo wanawake ili kujitokeza kushiriki katika kuchukua fomu za nafasi za udiwani, uwakilishi na ubunge ili waingie katika vyombo vya kutunga sheria kupitia kwenye majimbo yao na sio kutegemea nafasi za viti maalumu ambazo kwa muda mrefu zinaonekana haziwasaidii wanawake katika kujiimarisha na kuiingia katika ushindani.

 Alisema wizara ya jinsia ina wajibu wa kuwasaidia wanawake katika uongozi na kwa kusaidiana na wanaharakati mbalimbali wanaweza kuwainua wanawake wenzao ili wawe wengi kwenye uongozi.

 “Kwa miaka mingi nguvu, uwezo na majukumu ya wanawake ulikua ukibezwa lakini kwa sasa wanawake wananguvu ya kufanya mambo makubwa yanayostahiki”alisema. 

 Naibu Katibu mkuu Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar, D Mwanakhamis Ameir, alisema lazima wanawake wawe na malengo kwa sababu katika safari ya uongozi kuna changamoto nyingi ambapo malengo yatasadia kufikia jitihada za kufika katika kuwa viongozi lakini pia elimu ni kitu muhimu.

 Kwa upande wao washiriki wa mkutano huo, walisema kuwa bado mfumo dume umetawala katika jamii kwa kuwaona wanawake ni walezi wa familia badala ya kushika nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya kisiasa na kiserikali.

Comments